Hatuwezi kuelewa
utawa
tukidhani ni kitu kimoja: jina hilo linajumlisha maisha tofautitofauti.
Katika makala hii tunataka kufuata
historia
ya maisha haya katika
Ukristo
kama kitabu bora kilichoandikwa na
Mungu
siku kwa siku kadiri ya mpango wake wa
hekima
kwa ujenzi wa
Kanisa
lake takatifu kwa
karama
za kumshuhudia
Yesu
katika sifa na kazi zake mbalimbali.
Kuna hatua kuu nne zilipozaliwa aina mpya za utawa (hasa magharibi) bila ya kufuta zile zilizotangulia:
Mwanzo: ubikira na juhudi nyumbani
[
hariri
|
hariri chanzo
]
Kufuatana na mifano ya
Yesu Kristo
na
Bikira Maria
,
Agano Jipya
linatoa habari za wanaume na wanawake waliojinyima
ndoa
kwa ajili ya
ufalme wa Mungu
, kama vile mabinti wanne wa
Filipo mwinjilisti
waliokuwa mabikira na manabii (
Mdo
21:9). Hasa
mtume Paulo
aliwahimiza Wakristo wowote wanaoweza wafanye hivyo kama alivyofanya mwenyewe kwa kufuata shauri la
Bwana
(taz.
1Kor
7:25-34).
Mababu wa Kanisa
kuanzia
karne I
waliandika juu ya wanaume waseja wanaozungukazunguka ili kuhubiri, na juu ya mabikira ambao
utakatifu
wao unaonyesha Ukristo ulivyo bora kuliko ulimwengu wa
anasa
unaoliudhi Kanisa.
Nje ya
Dola la Kirumi
(
Mesopotamia
na
Persia
)
useja
ulitazamwa kama agano na Kristo la kuwafaa wote.
Polepole mabikira walianza kuorodheshwa na kukubaliwa na
askofu
na kukusanywa katika jumuia. Ilitokea vilevile kwa wanaume wa toba walioanzisha miundo kamili kuliko juhudi za nyumbani mwao, wakishika ufukara fulani wa hiari, mafungo, kujinyima vyakula mbalimbali, kukesha usiku, kuimba
Zaburi
na kusali kwa moyo.
Tofauti na hao walioishi katika mazingira ya kawaida, mwishoni mwa
karne III
huko
Misri
ulianza mtindo wa kukimbia ulimwengu hata kimakao.
Mmonaki
(kutoka neno la
Kigiriki
monos = mmoja) alitafuta
upweke
kamili hasa jangwani ili kuishi na Mungu tu, ili moyo uweze kutulia kabisa bila ya kushikwa na mitindo na masharti ya maisha ya kawaida. Miundo mipya ya umonaki ilitegemea matatu:
mwanzilishi
,
kanuni
, upweke.
Mtindo huo wa maisha, ambao ndio mchango mkuu wa
Afrika
kwa Kanisa lote, ulistawi hasa baada ya
Dola la Kirumi
kuruhusu Ukristo (
313
). Maisha hayo magumu, yaliyoenea mapema hata nje ya Dola hilo, yaliamsha waamini wafuate
Injili
kwa juhudi kama wakati wa dhuluma, ulipohitajika ujasiri mbele ya hatari ya kuuawa. Hivyo umonaki ulionekana aina mpya ya
kifodini
kwa jinsi ulivyomtolea Mungu maisha yote.
Anayeheshimiwa kama baba wa wamonaki ni
Antoni abati
(
251
-
356
) ambaye akizingatia maneno mbalimbali ya Injili aliwagawia maskini utajiri wake mkubwa amfuate
Mwokozi
. Maisha yake yote akazidi kujitafutia mahali pa upweke kamili zaidi ili kumlenga Mungu tu.
Mfano wake ulivuta wanaume na wanawake wengi toka sehemu mbalimbali aliowaongoza bila ya kuacha upweke wake, isipokuwa kwa kutetea
imani sahihi
na
umoja
wa Kanisa. Mara baada ya kifo chake kitabu kilichoandikwa na
Atanasi
(
295
-
373
) juu yake kikaeneza mvuto wa umonaki hadi magharibi.
Muda mfupi baadaye, na sehemu ileile, yalianzishwa maisha ya pamoja ambamo mali na vilevile mang’amuzi ya Kiroho yashirikishwe, hata kwa waamini wa ulimwenguni.
Pakomi
(
288
-
346
) aliongokea imani kwa kuzingatia Wakristo walivyowatumikia wafungwa kwa
upendo
. Mang’amuzi hayo ya awali yalimuangazia kuwa Mungu ni upendo yakaathiri maisha na mafundisho yake yote. Hivyo baada ya kushika umonaki akajisikia wito wa kuishi kwa upendo na wengine akaanzisha maisha ya pamoja upwekeni Misri Kusini. Ndiye wa kwanza kutunga
kanuni ya kitawa
, na ndani yake jina “ndugu” linashika nafasi ya “mmonaki”.
Kanuni hiyo ikaja kuathiri maisha ya wamonaki na kanuni zao mashariki na magharibi vilevile, na ndiyo inayoongoza umati wa wamonaki wa
Ethiopia
tangu mwaka
500
hivi. Mbali ya mafungo na
sala
ndefu, Pakomi alisisitiza kujikana kwa ajili ya wengine, yaani kuwa na
utiifu
,
huruma
na misaada ya kila aina: ndiyo njia ya upendo ambayo iliagizwa na Bwana na kufanya maisha ya pamoja yawe bora kuliko upweke kamili. Karibu na
monasteri
za kiume kulikuwa na nyingine za kike.
Pia
Bazili Mkuu
(
330
-
379
), baada ya kutembelea wamonaki sehemu mbalimbali, alianzisha maisha ya pamoja katika “jamaa” ambayo lengo lake kuu lilikuwa kushika kikamilifu
udugu
wa Kiinjili kama katika Kanisa la mwanzoni. Tofauti na monasteri ya Pakomi iliyofikia kuwa na maelfu ya watawa, jamaa hiyo haikuwa na idadi kubwa wala ngome; tena haikuwa jangwani, bali karibu na mji wa
Kaisarea wa Kapadokia
. Akiwa askofu huko alisisitiza uhusiano na Kanisa: watawa wa kiume na wa kike wawe
chachu
inayofanya Wakristo wenzao wafuate utakatifu wa
wito
wao; tena aliwakabidhi shughuli mbalimbali kama vile kuhubiri na hasa kuhudumia wenye shida. Mtindo huo ulisisitiza ushirikiano kati ya ndugu kuliko uongozi wa
abati
na miundo mikubwa. Pia ulitia maanani masomo ya kidini.
Mpaka leo kanuni zake zinaongoza karibu wamonaki wote wa mashariki, na kwa njia yao makanisa ya Orthodoksi kwa kuwa kwao maaskofu kwanza ni wamonaki nao wanaelekeza Wakristo wote kufuata mifano yao.
Katika nchi ya jirani
Mesrop
(
361
-
440
) akaanzisha mtindo wa monasteri kuwa na shule karibu ili kuandaa watu watakaoendeleza
elimu
ya dini hasa kwa kutafsiri na kunakili vitabu. Mapema monasteri kubwa zikawa pia na
seminari kuu
au vyuo vikuu vya
teolojia
.
Huo umonaki wa
Armenia
ulidumisha
utamaduni
wa taifa hilo, ambalo lilikuwa la kwanza kupokea Ukristo jumla pamoja na mfalme wake (
300
) halafu likaushika moja kwa moja hata lilipopitia vipindi vigumu sana.
Tangu
karne IV
umonaki ulienea magharibi pia: huko
Italia
,
Ufaransa
na
Hispania
kulikuwa na monasteri za kike na za kiume zilizosimamiwa na maaskofu watakatifu. Kati yao wa kwanza kupitia umonaki ni
Martino wa Tours
(
316
-
397
).
Hasa maandishi ya
Yohane Kasiano
(
360
-
435
) yalieneza hekima ya wamonaki wengi wa mashariki alioongea nao.
Augustino wa Hippo
(
354
-
430
),
babu wa Kanisa
muhimu kuliko wote, baada ya kuongoka na kutembelea baadhi ya monasteri, alirudi Afrika Kaskazini aanzishe maisha ya pamoja. Kwanza aliishi na walei wenzake, halafu akiwa askofu aliishi na mapadri wake, akawashirikisha utajiri wake wa
akili
na
roho
ili wafanye vizuri
utume
. Katika kanuni yake, iliyotumika kwa wanawake pia, umoja uliwekwa kuwa lengo lenyewe la utawa, si jambo lake mojawapo tu. Hata yeye aliathiri sana maisha ya kitawa ya magharibi kote.
Benedikto wa Nursia
(
480
-
547
) ndiye aliyeunda umonaki wa magharibi kwa namna ya kudumu hasa kwa njia ya kanuni aliyoitunga polepole, kutokana na mang’amuzi yake,
Kanuni ya Mwalimu
asiyejulikana na mafundisho ya Bazili na mababu wengine wa jangwani.
Kanuni yake iliunganisha vizuri maelekeo mawili ya umonaki wa zamani: kumtafuta Mungu kwa juhudi upwekeni na kuishi kwa umoja. Sifa yake nyingine ni mchanganuo mzuri wa
sala na kazi
mbalimbali ambazo ziliokoa elimu ya zamani na kufufua
uchumi
wa Ulaya Magharibi baada ya makabila ya Kijerumani kuvuruga kote. Yeye alidumisha ubaba wa Kiroho katika jumuia nzima: ndiyo maana abati ana nafasi ya pekee na ya kudumu kwa wamonaki, ambao aliwafafanua kuwa watu “wanaoishi katika monasteri na kutii kanuni moja na abati mmoja”. Kwake monasteri ni shule ya
utumishi wa Bwana
, ambapo abati ndiye mwalimu, na kanuni ndiyo kitabu. Kinyume cha watawa wazururaji wa zamani hizo za misusuko, Benedikto alidai udumifu katika monasteri.
Kutokana na kila monasteri kujitegemea,
Wabenedikto
wakapata sura tofautitofauti bila ya kuachana na kanuni. Ushirikiano kati ya monasteri mbalimbali unategemea asili yake na mitindo yake.
Kati ya aina nyingine za umonaki wa magharibi inakumbukwa hasa ile ya
Wakristo wa Kiselti
(
Ulaya
visiwani). Hao hawakuwa na majimbo bali walimtegemea
askofu-abati
wa monasteri ya jirani na kufuata desturi za kimonaki, hasa maisha magumu ya malipizi na maungamo ya mara kwa mara. Kutoka huko wamonaki wengi walihamia Ulaya bara kama wasafiri wa Kristo na wamisionari wakieneza desturi hizo. Kati yao anasifiwa hasa
Kolumbani
(
540
-
615
).
Hatimaye wakaja kukubali kanuni ya Benedikto pamoja na desturi za Kanisa la
Roma
.
Wamonaki wengine pia walichangia sana uenezaji wa Ukristo Ulaya, k.mf.
Augustino wa Canterbury
(+
605
), aliyetumwa
Uingereza
na
Papa Gregori I
(
540
-
604
), mmonaki wa kwanza kufikia Upapa, halafu
Bonifas
(
672
-
754
), mtume wa
Ujerumani
na
mfiadini
.
Ni kawaida ya
binadamu
kuanzisha kazi kwa nguvu halafu kuchoka, kuanza safari kwa kasi halafu kupunguza mwendo. Vilevile jumuia zina vipindi vya bidii na vya
ulegevu
.
Kanisa lenyewe, ingawa ni takatifu, linaathiriwa na
ukosefu
wa wanae. Ila
Roho Mtakatifu
haliachi bila ya msaada wa watu motomoto ili kulirekebisha.
Utawa unahusika kabisa na utakatifu wa Kanisa: ukistawi mmoja, unastawi wa pili pia. Hasa katika
karne IX
hadi
XII
Kanisa la magharibi
lilitambua wazi haja ya
urekebisho
katika umonaki na katika maisha yake yote.
Kati ya matawi mapya ya Kibenedikto yaliyotokana na juhudi hizo yanakumbukwa hasa lile la
Cluny
(ambalo lilikwepa kuwa mikononi mwa watawala likakazia
liturujia
kuliko kazi za mikono), lile la
Camaldoli
(lililofufua
ukaapweke
) na lile la
Citeaux
(ambalo lilirudia maisha magumu katika ufukara na kazi).
Wamonaki wa matawi hayo wakaja kushika nafasi muhimu katika kurekebisha Kanisa, hasa
Petro Damiani
(
1007
-
1072
),
Papa Gregori VII
(
1028
-
1085
) na
Bernardo wa Clairvaux
(
1090
-
1153
).
Wakati huohuo
Bruno
(
1035
-
1101
) alianzisha aina mpya ya ukaapweke iliyodumu kuwa na juhudi hadi leo (
Wakartusi
).
Ili kuboresha maisha ya mapadri wanajimbo, toka zamani ulisisitizwa uundaji wa jumuia kati yao, ambamo wasali na kufanya utume kwa pamoja.
Hasa kuanzia
karne XI
wengi walifanya hivyo kwenye makanisa makubwa kama mtindo mpya wa kitawa unaosisitiza liturujia ya fahari pamoja na
uchungaji
.
Inavyoweza kueleweka, hao walifuata kanuni ya Augustino na kuitwa Wakanoni. Maarufu zaidi katika yao ni
Norbert
(
1082
-
1134
), mwanzilishi wa
Wapremontree
.
Watawa askari, wanahospitali na wakombozi wa watumwa
[
hariri
|
hariri chanzo
]
Katika
karne XII
, ambapo baadhi ya Wakristo walipiga
vita vya msalaba
kuikomboa
nchi takatifu
, na baadhi walitekwa na Waislamu kuwa watumwa, zilianzishwa aina mpya za watawa ambao washike
maisha ya Kiroho
pamoja na upanga ili kusindikiza, kukaribisha, kulinda na kutibu waliohiji
Yerusalemu
, au wajitolee kukomboa watumwa hata kwa kubadilishana nao.
Baadhi ya mashirika hayo yanadumu mpaka leo, lakini yamebadili sana malengo na mbinu. Kati ya waanzilishi wakumbukwe
Yohane wa Matha
(
1154
-
1213
) na
Petro Nolasco
(
1180
-
1249
).
Kama kawaida bidii kwa urekebisho wa Kanisa zilifanikiwa kiasi tu: hasa walei hawakuridhika.
Pia
hija
na vita vya msalaba vilifanya wengi wajionee nchi ya Yesu na hivyo kuvutiwa upya na maisha yake. Ndiyo sababu walistawisha mifumo mbalimbali ya Kiinjili na kulenga maisha ya Kanisa la mwanzoni.
Dhidi ya mwenendo wa mapadri na wamonaki, walisisitiza ufukara na
unyofu
hata wengi walifikia hatua ya kuliasi Kanisa. Ulikuwa wakati wa utajiri kuzidi hata kufanya watu kadhaa waukinai.
Juu ya misingi hiyo katika
karne XIII
yalianzishwa mashirika mbalimbali (hasa
Wafransisko
na
Wadominiko
, lakini pia
Waaugustino
,
Wakarmeli
na
Watumishi wa Maria
) yaliyoitwa ya ombaomba kwa jinsi yalivyokaza ufukara.
Dominiko Guzman
(
1170
-
1221
) akiwa
padri
aliguswa na uenezi wa
uzushi
akajitahidi kutatua tatizo hilo. Ili akubaliwe na watu wote kama mhubiri halisi wa Injili alishika ufukara wa Yesu na
mitume
wake: kwenda wawiliwawili, kwa miguu, bila ya kuchukua chochote kwa safari. Hivyo aliliandalia Kanisa kundi la watu wanaofanya kazi ya kuhubiri, ambayo awali ilikuwa maalumu ya maaskofu. Kwa lengo hilo utawa wake ulipunguza miundo ya kimonaki na urefu wa liturujia ili kuacha nafasi ya kusoma na kusali zaidi mmojammoja: hivyo ndugu wahubiri watajipatia
ukweli
ambao wawashirikishe wengine kwa kuhubiri na kufundisha. Ndio utume unaolingana zaidi na maisha ya sala na kusoma.
Hata kuliko yeye, rafiki yake,
Fransisko wa Asizi
(
1181
-
1226
) alishikwa na hamu ya kulingana na Yesu kwa kufuata nyayo zake inavyofundishwa na Injili. Alifanya vilevile kazi ya kuhubiri, lakini bila ya kuzingatia elimu wala kubishana na wazushi, bali kwa kuelekeza njia ya toba kwanza kwa matendo halafu kwa maneno machache na manyofu. Kwa ajili ya Yesu alijinyima hata upweke alioupendelea, akawakaribia watu hasa wale wadogo zaidi.
Wafuasi wake hawakujifunga kuishi daima mahali fulani na watu walewale, bali walifungamana na jamaa ya kimataifa ambayo mkuu wake aweze kuwatuma popote. Hivyo iliwabidi wawe tayari kukabili mazingira yoyote na kushirikiana na ndugu mbalimbali. Tena udugu haukuishia shirikani bali ulitakiwa kuenea kwa watu na viumbe vyote. Kutokana na upya wa mtindo huo wa maisha, hata miundo yake ilipaswa kuwa mipya iweze kudumisha umoja wao.
Ufransisko ulilingana kikamilifu na madai ya urekebisho ya walei, pia uliwapendeza viongozi wa Kanisa walioona ulivyowarudishia utiifu wa waamini: hivyo ulienea kasi ajabu, hata kati ya wanawake na watu wa ndoa.
Watawa wa kike hawakuweza kufuata mtindo uleule: waliishi kimonaki lakini kwa kuzingatia ufukara na udugu wa Kifransisko na kwa kuombea utume wa hao ndugu wadogo.
Klara wa Asizi
(
1193
-
1253
), “mche mdogo” wa Fransisko, ndiye mwanamke wa kwanza kutunga kanuni ya kitawa. Tapo hilo ni maarufu kwa marekebisho yaliyofuatana hadi leo kuhusu ufukara.
Tangu
karne XII
wanawake wengine pia walichangia sana ustawi wa utawa, wa maisha ya Kiroho na wa Kanisa kwa jumla hata kwa maandishi yao. Kati yao
Katerina wa Siena
(
1347
-
1380
), wa
utawa wa tatu wa Mt. Dominiko
, ametangazwa kuwa
mwalimu wa Kanisa
.
Mashirika yasiyo na nadhiri za hadhara
[
hariri
|
hariri chanzo
]
Kuanzia
karne XIII
zilijitokeza pia jumuia nyingine ambazo pengine zinahusiana na mashirika ya kitawa (yaani za
Utawa wa Tatu
), lakini hazina
nadhiri
au si za hadhara. Kwa kuenea, zikaja kuwa na muundo kama wa mashirika (
1401
), ingawa kwa kawaida ya kwao yalikuwa na jumuia za kiume na za kike ndani yake.
Baada ya upinzani mwingi, wanawake wakaja kukubaliwa wafanye utume na kuanzisha mashirika yasiyobanwa na
ugo
. Kwa namna ya pekee
Anjela Merici
(
1474
-
1540
) alitaka wafuasi wake waishi na kutumikia kati ya watu; baada ya karne nne shirika lake likakubaliwa kutambulika kuwa la kilimwengu.
Upande wa wanaume
Filipo Neri
(
1515
-
1595
) ni maarufu kati ya walioanzisha jumuia ambapo watu wanaishi pamoja ili kujipatia
malezi
na kufanya utume fulani, lakini bila ya kuwekwa
wakfu
.
Karne XVI
ilidai sana urekebisho wa Kanisa lote. Katika jitihada hizo
Waprotestanti
walifikia hatua ya kujitenga, lakini wengine walirekebisha mashirika ya zamani: matokeo muhimu zaidi ni Ndugu Wadogo
Wakapuchini
(
1525
), halafu
Wakarmeli Peku
wa
Teresa wa Yesu
(
1515
-
1582
) na
Yohane wa Msalaba
(
1542
-
1591
).
Wengine walianzisha matapo mapya ya Kiroho na mashirika yanayolenga hasa utume, kwa kupunguza ukubwa wa nyumba na urefu wa sala za pamoja: pengine hayahitaji ratiba wala ushirikiano isipokuwa kati ya kiongozi na mtawa mmojammoja. Mashirika hayo hayana kanuni bali
katiba
tu.
Kati ya yote lile la Yesu (
Wajesuiti
) ndio muhimu zaidi. Mwanzilishi wake,
Ignas wa Loyola
(
1491
-
1556
), ambaye kabla hajaongoka alikuwa askari, alileta utawani mtindo wa kijeshi, akisisitiza utiifu kwa viongozi wa shirika na kwa
Papa
(baadhi wanajifunga kwake kwa
nadhiri ya nne
, nguzo kuu ya shirika). Hivyo Mjesuiti jumuia yake halisi ni shirika tu ambalo linaweza kumtuma kokote duniani, naye atafanya kazi yoyote kwa niaba ya shirika, tayari kukabili mazingira na hali yoyote.
Mashirika ya kutolea huduma maalumu
[
hariri
|
hariri chanzo
]
Baada ya mashirika ya namna hiyo yaliyolenga
wakleri
,
Yohane Batista de La Salle
(
1651
-
1719
) alianzisha la kwanza kwa ajili ya ma
bradha
tu, kwa lengo la kuendesha
shule
kwa
maskini
.
Halafu mashirika ya kike na ya kiume zaidi ya 2000 yalilenga
huduma
maalumu inayohitajika lakini haina wa kuitoa, k.mf. kuhubiri vijijini, kulea vijana, kufundisha ma
fukara
, kuuguza wagonjwa, kuanzisha
misheni
, kushughulikia
upashanaji habari
. Mara nyingi mashirika hayo yanafanana ingawa yalianzishwa wakati na mahali tofauti, kwa kawaida chini ya askofu wa
jimbo
na hasa katika
karne XIX
.
Kati ya waanzilishi muhimu zaidi wakumbukwe
Vinsenti wa Paulo
(
1576
-
1660
),
Alois Maria wa Montfort
(
1673
-
1716
),
Paulo wa Msalaba
(
1694
-
1775
),
Alfonso Maria wa Liguori
(
1696
-
1785
),
Karolo Yosefu Mazenod
(
1782
-
1861
),
Vinsenti Pallotti
(
1795
-
1850
),
Antoni Maria Claret
(
1807
-
1870
),
Yohane Bosco
(
1815
-
1888
),
Daniele Comboni
(
1831
-
1881
),
Arnold Janssen
(
1837
-
1909
). Kati ya wanawake,
Yoana Antida Thouret
(
1765
-
1826
),
Magdalena wa Canossa
(
1774
-
1835
),
Visensya Gerosa
(
1784
-
1847
) pamoja na
Bartolomea Capitanio
(
1807
-
1833
),
Fransiska Saveri Cabrini
(
1850
-
1917
), na hatimaye
mama Teresa
wa
Kolkata
(
1910
-
1997
).
Mashirika ya kilimwengu na jumuia mpya
[
hariri
|
hariri chanzo
]
Karne XX
, ngumu kwa Kanisa na kwa dunia yote, ilileta mang’amuzi mapya hasa katika maisha ya ulimwenguni. Kwa mara nyingine walei walichangia sana hali mpya ndani ya Kanisa, ya kuthamini na kushughulikia mambo ya kidunia.
Katika juhudi za kuratibu nyanja zote za maisha ya binadamu, baadhi walijisikia haja ya kuwekwa wakfu bila ya kujitenga na maisha ya kawaida. Polepole Kanisa likafikia uamuzi wa kuwakubalia (
1950
)
mashirika ya kilimwengu
ambayo waamini wanawekwa wakfu wawe chumvi, mwanga na chachu kati ya watu. Hivyo wanajitahidi kuwa na moyo wa kujikana na bidii ya kitume kama watawa, lakini pia utaalamu wa kisasa na urahisi wa kupenya mazingira yoyote kama walei.
Halafu
Mtaguso wa pili wa Vatikano
(
1962
-
1965
) uliagiza uanzishwe tena
utawa wa mabikira
ambao waishi ulimwenguni na kuwekwa wakfu kwa ajili ya jimbo, si kwa
shirika
lolote.
Nusu ya pili ya karne hiyo ilililetea Kanisa Katoliki neema za matapo mengi yaliyoanzishwa kwa kawaida na walei na kuenea kati ya watu milioni na milioni. Mbali ya watawa wengi kuyafuata na miito mingi kupatikana ndani yake, baadhi ya wafuasi wa matapo hayo hawaingii shirika fulani bali wanakusanyika kuishi kijumuia au kuwekwa wakfu katika matapo yenyewe ili wayaongoze Kiroho kwa kuchimba karama yake.
Wengine pia waliona haja ya kujumuika hata nje ya miundo ya kitawa, wakifuata mitindo ya kimonaki au kutoa huduma kwa wasiojiweza ndani ya jumuia, ingawa baadhi yao wana ndoa.
Muundo wa pekee ulikubaliwa kwa
Opus Dei
ambayo ina mapadri, seminari mbalimbali na walei popote duniani: ni kama jimbo lisilo na eneo maalumu. Mwanzilishi wake ni
Yosefu Maria Escriva
(
1902
-
1975
).
Mbele ya upya huo wote
sheria za Kanisa
siku hizi zinamhimiza askofu yeyote afanye utambuzi wa aina mpya za maisha yaliyowekwa wakfu zikijitokeza jimboni.
Utawa kati ya Wakristo wa madhehebu mengine
[
hariri
|
hariri chanzo
]
Pamoja na kudumisha moja kwa moja umonaki kati ya
Waorthodoksi
, Roho Mtakatifu ameongoza
Waprotestanti
kadhaa kuanzisha upya maisha ya kitawa baada ya babu zao kuyafuta kama kitu kinyume cha Injili.
Kuanzia mwaka
1836
katika nchi mbalimbali watu wa
madhehebu
hayo walianza tena kuishi kijumuia kwa kufuata pengine mapokeo ya Kibenedikto na ya Kifransisko.
Maarufu zaidi ni Jumuia ya
Taize
, ambayo ilianzishwa na ndugu
Roger Schutz
(
1915
-
2005
) na kupokea Wakatoliki pia; lengo lake hasa ni umoja wa Wakristo na kuinjilisha vijana.
|
Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni
mbegu
.
Je, unajua kitu kuhusu
Historia ya Utawa
kama historia yake, matokeo au athari zake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa
kuihariri na kuongeza habari
.
|